Features
December 06, 2021

Yara Tanzania Kushirikiana Na Serikali Kuhamasisha Matumizi Bora Ya Mbolea Na Ukulima Wa Kisasa.

Yara TZ
Yara TZ

KAMPUNI ya mbolea ya Yara Tanzania imesema itaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kuwa mkulima wa zao la pamba anaongeza uzalishaji na tija ili kuinua kipato chake na pia kuongeza malighafi ya pamba itakayotumika katika viwanda vya hapa nchini.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkulima wa Pamba katika Kata ya Miguwa, Wilayani Nzega Mkoani Tabora jana, Meneja Biashara wa Yara Tanzania, Philipo Mwakipesile alisema mafanikio hayo yataweza kupatikana endapo wakulima wa zao hilo watatumia kwa ukamilifu matumizi ya mbolea na kufuata kanuzi zote za ukulima wa kisasa.

Alisema Yara kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba Tanzania waliweka mashamba darasa 124 katika mikoa minne ya Simiyu, Mwanza, Tabora na Geita na wilaya zake 12 kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2020/21 ili wakulima wa zao la pamba waweze kujifunza kwa vitendo namna bora ya matumizi ya mbolea ya Yara huku kampuni hiyo ikitoa mifuko 31 ya mbolea ya kupandia na mifuko 31 ya mbolea ya kukuzia kwa mashamba darasa yote.

“Kampuni ya Yara ina furaha kubwa kuona kile ilichofanya kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba kimekamilika na ni matumaini yetu wakulima wamejifunza umuhimu wa kutumia mbolea ili kuupa mmea lishe linganifu hivyo kuongeza uzalishaji wa pamba kwa eneo.

“Hapa Miguwa tuliweka shamba darasa ekari moja lililotumia mbolea ya kupandia ya YaraMila Otesha (NPK 13:24:12) mfuko 1(50kg) na ya kukuzia kwa mbolea ya YaraBela Sulfan (CAN 24%N+6%S) mfuko 1(50kg) na ekari nyingine haikuwekwa mbolea kama kilimo cha wakulima wengi wa pamba wafanyavyo, ni matumaini yetu matokeo yake kama inavyooneka hapa yataleta hamasa kubwa kwa wakulima kutumia mbolea”, alisema.

Akizungumza mahali hapo, Meneja wa Kanda ya Magharibi wa Bodi ya Pamba, Jones Bwahama alisema bodi hiyo imepanga kuhamsisha ulimaji wa zao hilo la pamba kwa kutoa elimu ya wakulima juu ya kuzingatia kanuni bora za kilimo kwa kutumia mbolea na madawa vizuri na kupanda kwa nafasi zinazostahili ambapo itawawezesha wakulima kuvuna zaidi ya kilo 1000 kwa ekari moja.

Naye Ofisa kutoka katika Ofisi ya Kilimo Mkoa wa Tabora, Modest Kaijage alisema matumizi ya mbolea ni muhimu sana kwa mafanikio ya wakulima wa mkoa huo kwani utaleta tija kwa wakulima na kwa Taifa.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Miguwa, Anjelina Nyanda alisema mashamba darasa yaliyowekwa na Yara kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba katika kata hiyo yamewanufaisha wakulima wa kata hiyo kuacha kilimo cha mazoea na sasa kufanya kilimo chanye tija.

Mmoja wa wakulima wa Kata ya Miguwa, Mariam Mashala alisema amefurahishwa na matumizi ya mbolea ya Yara ya kupandia na kukuzia mahindi kwa kupata mavuno mengi kuliko awali hivyo anaomba mbolea hiyo iongezwe katika msimu ujao wa kilimo.
Meneja Biashara wa Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania, Philipo Mwakipesile,akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkulima wa Pamba kuhusu faida ya mbolea ya kupanda na kukuzia ya Yara katika eneo lililowekwa mashamba darasa kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba katika Kata ya Miguwa, Wilaya ya Nzega, Mkoani Tabora jana. 

Viongozi kutoka Kampuni ya Mbolea ya Yara na Bodi ya Pamba, viongozi wa kiserikali, wakuliwa na waalikwa wengine wakipiga picha ya kumbukumbu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkulima wa Pamba katika Kata ya Miguwa, Nzega, Tabora jana.

Meneja Biashara wa Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania, Philipo Mwakipesile (katikati, aliyevaa kofia), wakulima wa pamba na waalikwa wengine wakiangalia zao la pamba katika moja ya mashamba darasa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkulima wa Pamba kwenye eneo lililowekwa mashamba darasa hayo kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba katika Kata ya Miguwa, Wilaya ya Nzega, Mkoani Tabora jana.

Meneja Biashara wa Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania, Philipo Mwakipesile (katikati) akizungumza na baadhi ya wakulima wa pamba pamoja na waalikwa wengine wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkulima wa Pamba kuhusu faida ya mbolea ya kupanda na kukuzia ya Yara katika eneo walilowekamashamba darasa kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba katika Kata ya Miguwa, Wilaya ya Nzega, Mkoani Tabora jana. Wa tatu kushoto ni Meneja wa Kanda ya Magharibi wa Bodi ya Pamba Tanzania, Jones Bwahama.