Features
April 04, 2024

Mjane alivyokuza kipato shambani kupitia mpango wa kidigitali kutoka Yara Tanzania.

Monica ambaye ni mjane analima mpunga chini ya mpango wa kidigitali kutoka Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania unaowajengea wakulima uwezo


Mjane alivyokuza kipato shambani na kuimarisha familia kupitia mpango wa kidigitali kutoka Yara Tanzania.

Moshi. Mpunga ni miongoni mwa zao muhimu la chakula hapa nchini na limekuwa  likilimwa zaidi katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Mwanza na baadhi ya maeneo katika Mkoa wa Kilimanjro.

Kilimo hiki cha mpunga kimekuwa kimbilio la wakulima kutokana na umuhimu wake katika jamii. Licha ya kwamba zao hilo limekuwa likitegemea kilimo cha umwagiliaji, limekuwa ni mkombozi hasa kwa wakulima wanawake kwa kuwainua kiuchumi.

Katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo zao hili hulimwa zaidi  katika maeneo ya chekereni, Mabogini na baadhi ya maeneo ya wilaya za Same, limechangia kwa kiasi kikubwa kuinua vipato vya wanawake ambao wamejikita katika kilimo hicho.

Ikiwa leo ni siku ya kusherehekea siku ya wanawake duniani tunamwangazia Monica Paul Kilombe (55), mkazi wa kijiji cha Chekereni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambaye ameelezea namna ambavyo kilimo hicho kimeinua maisha yake.

Monica ambaye ni mjane analima mpunga chini ya mpango wa kidigitali kutoka Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania unaowajengea wakulima uwezo wa kulima mazao mbalimbali kisasa na kwa faida kubwa.  

Mpango huo wa kidigitali wa AfricaConnect ni ubunifu wa Yara Tanzania katika juhudi za kumkomboa wakulima wadogo na wa kati dhidi ya kadhia nyingi ambazo huwafanya wengi wo kumudu kilimo. 

Meneja wa huduma ya kidigitali wa Yara Tanzania na Rwanda Deodath Mtei anasema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022, jukwaa la AfricaConnect limewanufaisha wakulima kwa mikopo nafuu ya pembejeo, huduma za ugani na viatilifu, bima ya mazao na soko la uhakika kwa mazao yao kupitia usajili wa simu ya kiganjani.

Mtei anasema mpango huo kwa sasa unawanufaisha wakulima wa mahindi, mpunga, viazi mbatata, miwa na sunflower. Mwaka jana AfricaConnect ililenga kuwafikia wakulima zaidi ya 300,000. “Lengo letu ni kusajili wakulima milioni moja kufikia mwaka wa 2025,” anasema Mtei.  

Monica ambaye ni mjane aliyeweza kupambana kwa kusomesha watoto wake wanne kupitia kilimo hicho pamoja na kujenga nyumba ya kisasa ya kuishi.

Mama huyo  ambaye mume wake alifariki miaka 10 iliyopita ameweza kupambana katika kilimo hicho na kuweza kujikwamua kiuchumi pamoja na kuweza kufanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

Monica anasema huduma ya AfricaConnect kutoka Yara imemletea mageuzi makubwa katika kilimo chake bila kuhangaika kama hapo zamani. “Uzuri wake ni kwamba ukishajisajili, unapata huduma zote muhimu unazohitaji kwendeleza kilimo chako. Mpango huu umenirahisishia kuwafikia wawezeshaji wote katika mnyororo mzima wa kilimo cha mpunga kuanzia shambani hadi sokoni,” anasema Monica. 

Mwanzoni wa mwaka huu 2024, Monica alipata fursa ya kuwakilisha sauti ya wakulima katika kikao maalum cha mtandao cha Shirika la Biashara Duniani (WTO) kutetea hoja ya nchi wanachama kutoa nafuu ya kikodi na kisera kwa huduma za kidigitali na biashara kupitia huduma za intaneti ili kuwafikishia wakulima wengi kama yeye mahitaji yao ya kilimo kwa unafuu zaidi.

 Akielezea namna ambavyo kilimo hicho kimemnufaisha, anasema anao uzoefu wa miaka 10 na kwamba kipindi cha nyuma alikuwa analima bila mafanikio kutokana na kutokuwa na elimu sahihi ya kulima kilimo bora.

Ansema baada ya wakulima wa mpunga wa eneo hilo kuingia kwenye mpango maalumu wa programu ya Yara, wameweza kulima kwa tija kutokana na kuzingatia kanuni bora za kilimo wanazopewa na kampuni hiyo.

Anasema kabla ya kuingia katika programu hiyo, kwa zaidi ya miaka 10 walilima kwa shida na wakipata mavuno kidogo kwa msimu kwa sababu walikuwa hawana  pembejeo za kutosha kutokana na kukosa mikopo.

"Hiyo miaka 10 nimelima kwa shida sana bila kupata mkopo wa aina yoyote. Nilikuwa nalima tuu kwa shida na nilikuwa sifanikiwi lakini baada ya kuingia kwenye mpango wa 'Africanconnect' tulikopeshwa wakulima wadogo, ambapo tulipewa mbolea na wataalam (mabwana shamba) ambao wamakeuwa wakitutembelea kila mara."

Anasema kwa misimu mitatu sasa chini ya mpango huo ameona tofauti. Nimepata faida kubwa sana kwa sababu sasa hivi tunalima kwa tija kwani wataalam tunawapata mashambani na tunapata elimu tosha ya jinsi ya kutumia mbolea na kupiga dawa kwa wakati."

"Tangu nipate mkopo huu nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Licha ya kuwa mjane, nimeweza kujenga nyumba ya kisasa na kupeleka wanangu shule na mpaka sasa naendelea vizuri na maisha yangu bila wasiwasi wowote," anadokeza Monica. 


Alivyonufaika na Africaconnect

Anasema kabla ya kujiunga na mpango wa Africaconnect alikuwa akilima kimazoea na kutumia mbegu ile ile ya mavuno yake kuirudisha shambani hali ambayo ilidhoofisha mazao yake.

"Nilikuwa sijui kutumia mbegu bora, nilikuwa nikishavuna naweka tuu mpunga wangu alafu huo huo baadaye nakuja kuotesha, kwa hiyo nilikuwa siwezi kupata mazao bora yenye tija sokoni." Anawaasa wakulima wenzake kuhakikisha wanajiunga na Africaconnect kwani amejionea kilimo kinalipa kuliko baiashara nyingine yote.

"Baada ya mume wangu kufariki, niliona maisha yangu ndio yameishia hapo lakini nilipambana kwa kuamini kwamba nina watoto wadogo ni lazima wale lakini pia wasome, hivyo nilipambana mpaka hapo tulipokuja kupata wadau wa Yara Tanzania ambao wametusaidia kutukopesha pembejeo za kilimo na kutuletea karibu watoa huduma wengine katika kilimo."

Monica anasema huko nyuma alikuwa akivuna magunia 12 hadi 15 ya mpunga kwenye ekari moja. Lakini baada ya kuingia katika programu hiyo alipata mbegu bora na za uhakika ambazo zilimsaidia kupata mavuno mengi zaidi.

"Baada ya kujiunga na hii programu ya Yara Tanzania ninapata wastani wa gunia 18 hadi 22 kwenye ekari moja peke yake. Nawashauri wakulima wenzangu ambao hawajajiunga na mpango huu wa kidigitali wasichekewe maana ni mzuri na hasa unatusaidia sisi wakulima wadogo, maana manufaa yake ni makubwa."


"Sasa hivi nimepiga hatua kubwa sana za kimaisha na nimeweza kujenga nyumba yangu ya kisasa kupitia kilimo hiki, hapa nilipo mume wangu alishafariki, nipo mwenyewe lakini nimeweza kuisaidia familia yangu kutokana na kilimo hiki ambacho nafanya," 


"Ndani ya miaka miwili nimeweza kuongeza shamba kutoka ekari moja niliyokuwa nayo mpaka kufikia ekari 3 ambapo nina uwezo wa kutoa magunia 54, kwa manufaa haya ambayo nimeyapata nimeweza kuendesha maisha yangu mwenyewe, watoto wangu wanakula na kwenda shule vizuri na sasa hivi namiliki nyumba ya kisasa,"

Anasema kutokana na kwamba analima kilimo chenye tija, kwa sasa ana uwezo wa kupata kilo 105 hadi 110 za mchele kwenye gunia moja la mpunga.

Matamanio yake

 

Anasema kwa sasa anatamani kuwa mkulima mkubwa na anayelimiki mashamba makubwa wilayani hapa kwa kuwa tayari elimu anayo ya kutosha na  uwezeshaji wa kutoka kampuni ya Yara Tanzania.

"Natamani kupiga hatua kubwa zaidi ya hapa nilipo kikubwa tunaomba kampuni ya Yara iendelee kutuwezesha sisi wakulima wadogo ili tuweze kupiga hatua kubwa za kimaisha na natamani kufika mbali zaidi ya hapa,"

 

Mwisho

 

USULI: KUHUSU AFRICACONNECT

 

Africa Connect ni jukwaa la kidigitali linalotoa suluhisho la moja kwa moja na jumuishi kwa wakulima kupata ufadhili, mbolea bora, pembejeo zingine zote, huduma za ugani, bima ya mazao na soko linalopatikana kwa urahisi la mazao yao kupitia simu ya mkononi.